Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imetoa waraka uliojumuisha mambo mbalimbali katika jamii huku ikiwataka viongozi kutenda haki, kutokuwa na upendeleo, kuheshimu Katiba na sheria za nchi ya Tanzania.
Waraka huo ulisambazwa Alhamisi hii katika vyombo vya habari, ukiwa umetiwa saini na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania (KAT), Dk. Jacob Chimeledya.
Wengine ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian Tanzania (KMT), Dk. Isaac Nicodemo na Askofu Mkuu wa Kanisa la African Inland Church in Tanzania (AICT), Silas Kezakubi.
“CCT inatoa maelekezo kwa Wakristo wa makanisa wanachama na Watanzania wote kwa ujumla, kuendelea kulinda na kuheshimu misingi ya haki za binadamu na kuliombea taifa na viongozi wake ili waendelee kuwa na hofu ya Mungu na waadilifu. Watende haki, wasiwe na upendeleo na waheshimu na kuwa walinzi wa Katiba na sheria za nchi kama walivyoapa,” ulisema sehemu ya waraka huo.”
Aidha CCT ilieleza pia kusikitishwa na vitendo vya ujambazi na matumizi ya silaha katika jamii na kukemea matukio ya ukatili na yale ya watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Inasikitishwa na vitendo vya ujambazi na matumizi ya silaha katika jamii yaliyofikia kiwango cha kuua askari polisi.
Pamoja na hayo CCT inakemea matukio ya ukatili unaondelea katika jamii huku ikisema yapo matukio ambayo yamedhihirisha ushirikiano hafifu kati ya polisi na wananchi na kuendelea kujitokeza kwa matukio yanayoashiria chuki za kidini na kikabila.
Sambamba na hayo yote CCT ilizungumzia madawa ya kulevya : “Ili vita dhidi ya dawa za kulevya ifanikiwe, ni muhimu Serikali ikalenga kutokomeza kiini cha tatizo kwa kuwapata wahusika wakuu wa biashara hiyo bila kujali wasifu wao na nafasi walizonazo katika jamii. Serikali izingatie misingi ya sheria, haki na usawa katika kuwakamata, kuwapekua na kuwafikisha katika vyombo vya sheria bila kuonea mtu wala kusukumwa na misingi yoyote ya imani au itikadi ya mtu.
“Ni muhimu kwa Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kupata ajira na kuendesha shughuli za ujasiriamali ili kujiepusha na vitendo viovu vikiwemo matumizi ya dawa za kulevya na unywaji wa pombe kali. CCT inayaelekeza makanisa, wanachama, wazazi na walezi kuendelea kuwalea vijana wao katika misingi ya kidini ili wasijiingize katika matumizi ya dawa za kulevya na pombe kali.
Hata hivyo maaskofu hao walisema akati huu wa Kwaresma, tunawaombea na kuwaomba wale wote ambao kwa njia moja au nyingine wanajihusisha na dawa za kulevya au unywaji wa pombe kali, watubu na kuyaacha maovu yao na Mungu atawarehemu
Kuhusu hali ya chakula hali ya chakula nchini CCT waliiomba Serikali kupitia idara yake inayohusika, iratibu na kusaidia utekelezaji wa jambo hili, ili wananchi waweze kumudu bei, mfano mahindi hayo yakisambazwa, bei ishuke kutoka zaidi ya Shilingi 100,000 ifikie angalau Shilingi 60,000. Ilisema kuwa pamoja na mvua kuanza kunyesha, Serikali na wengine wawezeshe usambazaji wa chakula kutoka mikoa yenye ziada kwenda mikoa yenye uhaba wa chakula ili bei ya chakula iweze kushuka.
Katika suala la Elimu waraka huo ulisema pamoja na nia njema ya Serikali kutoa elimu bure, lakini iangalie masilahi ya walimu na kuwe na mpango mkakati unaotekelezeka wa kuimarisha miundombinu ya kufundishia.
Jumuiya hiyo imewataka Watanzania kwa ujumla kuliombea taifa na viongozi wake, ili wawe walinzi wa Katiba na sheria za nchi kama walivyoapa.
0 comments:
Post a Comment