WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dk Joyce
Ndalichako, amesema atafuatilia shule za Serikali ili kujua sababu za
kufanya vibaya katika mitihani yao. Dk Ndalichako ambaye aliwahi kuwa
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta), amesema hayo jana baada
ya kuapishwa na Rais John Magufuli, kushika wadhifa huo.
“Kwa kuwa lengo langu ni kuona elimu bora inatolewa, nitafuatilia
kujua sababu ya shule maalumu za Serikali kushuka kiwango chake katika
ufaulu wa mitihani,” alisema. Kwa mujibu wa Dk Ndalichako, shule hizo za
Serikali hasa za vipaji maalum, ndizo awali kila mwanafunzi alipenda
kwenda kusoma tofauti na sasa ndio maana anataka kujua kulikoni.
Shule hizo ni pamoja na Mzumbe, Ilboru, Tabora Wavulana, Tabora
Wasichana, Kilakala na Msalato. Ada holela, kukaa chini Kuhusu upandaji
holela wa ada za shule binafsi, Dk Ndalichako alisema atapambana na vyuo
vikuu na shule binafsi, zinazofanya ujanjaujanja wa kupandisha ada
tofauti na ile iliyoandikwa kwenye barua za kuwaita wanafunzi, jambo
linalosababisha usumbufu kwa wazazi.
Alisema lengo lake ni kuhakikisha Tanzania inatoa elimu bora kwa
wahitimu wa vyuoni na sekondari, itakayowawezesha kukidhi soko la ajira
la kimataifa. Pamoja na ubora huo, Dk Ndalichako alisema ataangalia
uwepo wa miundombinu kwa wanafunzi wa kuanzia shule ya msingi na
sekondari, ambako alikiri kuwa baadhi ya wanafunzi wanaketi chini na
wengine wana matatizo ya mashimo ya vyoo.
“Inakuwaje shule yenye maelfu ya wanafunzi watumie shimo moja la
choo, haya na mambo mengine yanakwaza wanafunzi wasipende shule na
wengine wakatize masomo yao. “Tunataka kuandaa mwanasayansi, hivi kweli
mwanafunzi anayeketi chini anaweza kuwa mtaalamu mzuri wa sayansi? Ni
lazima tuwezeshe shule zetu ziwe na miundombinu rafiki kwa wanafunzi,”
alisema Dk Ndalichako.
0 comments:
Post a Comment