TAARIFA ZA KIMICHEZO KUTOKA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TFF
TFF BADO YASISITIZA KUMUONA WAZIRI MUKANGARA
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amemshukuru Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara kwa kukubali ombi la
Shirikisho la kutaka kukutana naye kwa mazungumzo na kumsihi asitishe
hatua anazodhamiria kuchukua hadi hapo kikao hicho kitakapofanyika.
Waziri Mukangara ameiagiza TFF
kuitisha Mkutano Mkuu wa marekebisho ya katiba ifikapo tarehe 15 Aprili
2013 na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi ifikapo tarehe 25 Mei 2013 na kwamba
tamko la TFF kutekeleza maagizo hayo liwe limetolewa katika muda wa siku
tano zinazoishia Jumatatu (Machi 11, 2013).
Katika barua pepe ambayo
amemuandikia Waziri ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi, Rais Tenga
ameeleza kuwa alikwenda ofisini kwake tarehe 7 Machi 2013 kujaribu
kumuona lakini akaambiwa amesafiri, hivyo kuomba kukutana na Katibu Mkuu
wa Wizara, ambaye pia hakuwepo ofisini na hatimaye akakutana na Naibu
Katibu Mkuu.
Katika barua hiyo pepe, Rais
Tenga ameeleza madhumuni ya kutaka kuonana na Waziri Mukangara kuwa ni
kwanza “kukushukuru kwa kukubali kuonana na ujumbe wa TFF ulioongozwa na
mjumbe wetu wa Kamati ya Utendaji, Bw. Alex Mgongolwa, akiongozana na
Katibu Mkuu wa TFF, Bw. Angetile Osiah, jana tarehe 6 Machi 2013.
“Kukushukuru kwa kukubali kukutana nasi tena siku ya tarehe 19 Machi, kwa ajili ya mazungumzo juu ya maagizo yako.
“Kukuarifu kuwa nimepokea maagizo yako uliyoyatoa jana kupitia kwa Mjumbe wetu wa Kamati ya Utendaji na kwa njia ya barua; na
“Kwa heshima na taadhima, kukuomba usitishe hatua yoyote ile
unayodhamiria kuchukua hadi hapo tutakapokutana na kupata maelezo yetu,
TFF, juu ya maamuzi na maagizo uliyoyatoa.”
Tenga, ambaye ni mjumbe wa Kamati
ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) aliondoka
jana (Machi 7 mwaka huu) kwenda Marrakech, Morocco kuhudhuria kikao cha
kamati hiyo na pia Mkutano Mkuu wa CAF ambao umepangwa kufanyika Machi
10 mwaka huu ukihusisha pia ajenda ya uchaguzi wa rais.
0 comments:
Post a Comment