
BAADA ya kuishi nchini Canada kwa zaidi miaka miwili sasa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa amesema anakuna kichwa ili kupima mazingira yaliyomfanya aondoke nchini na familia yake kama yapo au laa.
Septemba,2015
wakati wa Uchaguzi Mkuu Dk. Slaa alijiweka kando na siasa, kwa kile
alichokieleza kutofautiana na chama chake juu ya masharti ya kumpokea
aliyekuwa mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),Edward
Lowassa.
Hata
hivyo Dk. Slaa ambaye amekuwa mbunge wa Karatu kwa vipindi vitatu
mfululizo, hakuweza kuainisha mazingira yaliyomfanya aondokea nchini na
kwenda kuishi ughaibuni.
“Sina
tabia ya kuyumbishwa…sina chuki na mtu yeyote, sipendi siasa za
udanganyifu na propaganda. Nimeachana na siasa tangu Julai 28,2015,
baada ya kuona misingi ya chama nilichoshiriki kukijenga
imepotoshwa,”alisema Dk. Slaa siku alipotangaza kuachana na siasa.
Pamoja
na mambo mengine, alisema sharti la kwanza ambalo alitaka Chadema
izingatie ni kiongozi huyo wa zamani ndani ya serikali ya CCM,
kujisafisha dhidi ya tuhuma ya kashfa ya sakata la Kampuni ya Kufua
Umeme ya Richmond aliyohusishwa nayo akiwa Waziri Mkuu.
Kurudi nchini
Akizungumza
na MTANZANIA akiwa nchini Canada jana, Dk. Slaa alisema amemaliza
masomo yake na baada ya kufanya tafakari atarejea nchini wakati wowote.
“Ni
kweli nimemaliza masomo yangu. Bado napima mazingira yaliyonifanya
niondoke na familia yangu. Baada ya hapo tutaangalia uwezekano wa
kurejea,”alisema.
Alisema kuhusu matarajio yake ya kisiasa, watu wameshindwa kumwelewa siku ambayo alitangaza kustaafu siasa za vyama.
Alisema
alichomaanisha ni kwamba, pamoja na kuachana na siasa za vyama,atakuwa
tayari kupiga kelele pale anapoona masilahi ya Taifa yanaumia.
“Hadi
sasa sijapiga kelele kwa kuwa sijaona masilahi ya Taifa yakiangamizwa,
hatua mbalimbali zinazochukuliwa ni kweli zinawaumiza wasiohusika.
“Ndio
maana nilitumia katika makala mojawapo mtego wa panya huwakamata
wanaohusika na wasiohusika. Hivyo, makosa madogo mimi hayanisumbui kwa
kuwa hakuna binadamu kamilifu ,”alisema.
Rais Magufuli
Akizungumzia
utendaji wa Rais Dk. John Magufuli, alisema watu waelewe hakuna nchi
hata moja ambapo kiongozi atakubalika na watu wote kwa asilimia 100.
Alisema wako watu ambao masilahi yao yataguswa kwa namna moja au nyingine hivyo lazima watapiga kelele.
Kutokana
hilo, alisema Rais Dk. Magufuli katika kundi ambalo halihitaji fedha
ameyatekeleza yote kwa asilimia 99.9, ikiwa ni pamoja na uwajibikaji
serikalini, kuchukua hatua kali dhidi ya rushwa, uwizi wa mali za umma,
uwindaji haramu na kudhibiti dawa za kulevya.
“Hatua
zote zimechukuliwa,zinapaswa kuwa endelevu. Kwa bahati mbaya mchwa
wengine waliopenya mpaka ndani ya Ikulu na Serikali na huwezi kufagia
Serikali nzima kwa siku mmoja.
“Kwa
jinsi Rais ambavyo hayumbi na wala hayumbishwi, nina hakika atafikia
malengo na kurudisha Taifa kwenye misingi ya tunu za Taifa ya uwazi,
ukweli, uadilifu, kuheshimiana na kuthaminiana na hasa kujali utu.
“Hii
ndiyo hali ambayo JPM kila siku anaiita ‘Transition’ (kipindi cha
mpito). Tutafika tu, tunatakiwa kuwa wavumilivu na wenye uzalendo wa
kweli ana nia njema ya kufikisha Taifa mahali pazuri. Hii inahitaji
kuweka pembeni maslahi yetu binafsi kama mtu mmoja mmoja, viongozi wa
Serikali au hata wa kisiasa,”alisema Dk. Slaa.
Upinzani
Kuhusu
mwenendo huo endapo utasaidia upinzani kuingia Ikulu 2020, Dk. Slaa
alisema wakija na ajenda mbadala na makini yenye kuwalenga wananchi moja
kwa moja itawasaidia.
Dk.
Slaa ambaye pia alipata kugombea urais kupitia Chadema mwaka 2010,
alisema endapo wataendelea kurukia kauli za Rais, basi upinzani
utafutika kabla ya 2020.
“Kama
nilivyorejea mara kadhaa, upinzani makini utaingia Ikulu kwa ajenda
mbadala. Ajenda makini yenye kuwalenga wananchi moja kwa moja katika
kuwatoa kwenye kero zao mbalimbali.
“Hadi
sasa ninachoona ni ‘kurukia’ kauli za JPM, lakini kauli si ajenda na
hatupeani maksi kwa kuzungumzia usahihi wa lugha. Wako wanaotazama
usahihi wa lugha na mahali pa kutazama usahihi huo. Kimsingi hayo ni
masuala ya darasani au kwenye uandishi wa vitabu.
“Aidha
kumtuhumu JPM kukiuka Katiba na sheria nayo haina tija. Wote
wanaomtuhumu wanajua kuwa wakiambiwa waonyeshe kifungu mahususi
alichokiuka yeye mwenyewe katika utendaji wake hawana majibu ya
kuridhisha.
“Hivyo
mimi sijaona mwenendo wa JPM unaosaidia kuingiza upinzani Ikulu.
Isitoshe kama hawatakuja na ajenda makini na mkakati ulioandaliwa
unaowatoa wananchi hapa walipo kwenda kwenye raha, upinzani unaweza
kufutika kabla ya 2020,”alisema Dk. Slaa.
0 comments:
Post a Comment