Posted by Williammalecela.com on Tuesday, October 04, 2016
KAMANDA
wa Polisi Kanda Maalum ya Mkoa wa Dar es Salaam, Simon Sirro amesema
jeshi hilo limemkamata mtuhumiwa ‘Scopion’ aliyehusika katika matukio ya
unyang’anyi wa kutumia silaha eneo la Buguruni jijini humo. Sirro
alitoa kauli hiyo jana Buguruni kwa Mnyamani jijini Dar es Salaam wakati
wa mkutano wa kujadili usalama katika eneo hilo ulioandaliwa na Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.Alisema mtuhumiwa huyo
anayejulikana kwa jina maarufu kama Scopion alikamatwa baada ya polisi
kupewa taarifa za matukio ambayo ameyafanya ikiwemo la kumchoma kisu,
kumtoa macho na kumsababishia upofu, Said Ally. "Nimesikia wananchi
wanalalamika hapa kuwa tumeshindwa kumkamata Scopion, ni nani kwa Jeshi
la Polisi asikamatwe, tayari tumemkamata na sheria itachukua mkondo
wake, hakuna mtu anayeweza kushindana na jeshi," alisema. Aidha Sirro
alisema baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo na kuhojiwa aliutaja mtandao
wake wote na tayari wameukamata, hivyo amewataka wakazi wa eneo hilo
kutokuwa na hofu kwani mtuhumiwa huyo hayupo tena katika eneo hilo.
"Najua suala hili bado lipo mahakamani hatuwezi kulizungumzia sana,
bahati nzuri alipokamatwa alieleza aliyoeleza na tukafanikiwa kuukamata
mtandao wote, hivyo hakuna haja ya kuwa na uwoga eneo hili lipo salama,"
alisema. Kabla ya kauli hiyo ya Sirro, wananchi wamelalamikia askari wa
eneo hilo ambao walishindwa kuchukua hatua kwa mtuhumiwa huyo ambaye
alikuwa akifahamika muda mrefu. Sadiki Mgaya ambaye alishuhudia tukio la
kuchomwa kisu na kutolewa macho kwa Said Ally, alisema mtuhumiwa huyo
alisema kuwa amekuja kwa ajili ya kulipa kisasi kwa wakabaji baada ya
yeye kukabwa. Alisema baada ya kufanya tukio hilo, askari walifika
katika eneo hilo na mtuhumiwa huyo akiwa hapo na wananchi waliwaonesha
askari lakini hawakuchukua hatua zozote badala yake waliwataka wananchi
wamkamate. Aidha wananchi hao pia wamemlalamikia Mkuu wa Kituo cha
Polisi Mnyamani na kudai kuwa amekuwa akipelekewa taarifa za uhalifu
ikiwemo za vibaka lakini mtu anapokamatwa akifika kituoni hapo anatoa
rushwa na kuruhusiwa kuondoka. Lakini akiondoka askari wengine wanatumwa
tena kumkamata. Kauli hizo za wananchi zikamfanya Sirro kutoa kauli
ambapo alisema askari na maofisa wote ambao wanashindwa kutimiza wajibu
wao watachukuliwa hatua ikiwemo kufikishwa mahakamani pamoja na
kufukuzwa kazi.
"Najua wapo askari na maofisa wa ovyo ambao hawajui
kutimiza wajibu wao, lakini nikuahidi Mkuu wa Mkoa tutawachukulia hatua,
nimesikia hapa wananchi wanalalamika askari wanachukua rushwa,
tutachunguza tukijiridhisha basi ni lazima tuchukue hatua," aliongeza.
Aidha
Sirro alisema watafanya doria kubwa katika eneo hilo ili kuwakamata
wote wanaohusika na matukio ya kihalifu kwani wamebaini katika eneo hilo
bado kuna uporaji mdogo mdogo.
"Tutarudi hapa tunaomba ushirikiano
wenu bila ninyi kutuambia hatuwezi kujua, nawaomba wazazi muwakanye
watoto wenu ambao wanahusika na matukio hayo kwani tutakapoanza msako
huo wasije wakalalamika, uhalifu haulipi na mwisho wa siku utamkosa
mtoto wako," alisisitiza.
Kwa upande wake Makonda aliwataka wananchi
hao kujitolea kufanya ulinzi shirikishi na kuwataka wananchi kuchangia
ulinzi huo ili vijana hao wahusike kufanya ulinzi na kulifanya eneo hilo
libaki na amani.
"Tuna wajibu wa kufanya ulinzi shirikishi wananchi
mtoe michango, hapa Sirro amesema mapungufu yaliyopo kwenye vituo
yanafanyiwa kazi, niwaase tu mjiepushe na matukio ya kuhalifu kwani wale
watakaokamatwa sheria itachukua mkondo wake," alisema Makonda.
Imeandikwa na Sophia Mwambe-Habarileo
Kama Una Habari,Picha,Tangazo n
0 comments:
Post a Comment