Salum
Henjewele (34) maarufu kama ‘Scorpion’ mkazi wa Yombo Machimbo
anayetuhumiwa kumchoma kisu na kumtoa macho, Saidi Mrisho jana
aliwashangaza watu kwa kufanya vituko mahakamani.
‘Scopion’ ambaye ni mwalimu wa mashwati
(karate) anadaiwa alifanya tukio hilo Septemba 6 mwaka huu eneo la
Buguruni Sheli Jijini Dar es Salaam.
Katika hali ya kushangaza, mtuhumiwa
huyo alibadilisha mavazi yake akiwa mahakamani, ili asijulikane mbele ya
umati wa watu waliokuwa wamefurika mahakamani hapo. Akiwa anatoka
mahakamani ‘Scorpion’ alionekana amevaa nguo tofauti na zile alizokuwa
amevaa asubuhi wakati kesi yake ikitajwa.
Awali mtuhumiwa huyo alivaa fulana
nyekundu na suruali ya jeans ya bluu, tofauti na mchana ambapo
alionekana amevalia baragashia kichwani na shati la mikono mirefu lenye
rangi ya kijivu. Mavazi hayo yaliwachanganya baadhi ya watu waliokuwa na
shauku ya kutaka kumwona akipanda gari la magereza. Hata hivyo
waandishi wa habari na wapiga picha walishtukia ‘janja’ hiyo na
kumtambua kwa haraka.
Awali, Scorpion alipandishwa kizimbani
mbele ya Hakimu Mkazi, Adelf Sachore kwa kuongozwa na Wakili wa
Serikali, Munde Kalombola kwa ajili ya kutajwa kwa shauri la unyang’anyi
wa kutumia silaha na kumsababishia upofu wa kudumu, Said Mrisho kwa
kumtoboa macho.
Hata hivyo shauri hilo liliahirishwa
hadi Oktoba 19 mwaka huu litakapotajwa tena. Kwa mujibu wa hati ya
mashtaka ya kesi hiyo namba 276 ya mwaka 2016 ilitajwa kwa mara ya
kwanza Septemba 28, mwaka huu. Hata hivyo mshtakiwa huyo jana alionekana
mtu asiye na wasi wasi, huku akitabasamu muda wote.
Katika hati hiyo ya mashtaka, ilidaiwa
kuwa, Septemba 6 mwaka huu saa 4 usiku maeneo ya Buguruni Sheli Wilaya
ya Ilala Dar es Salaam, aliiba cheni ya Silva yenye uzito wa gramu 34
ikiwa na thamani ya Sh 60,000 na black bendi ya mkononi pamoja na fedha
taslimu Sh 330,000 vyote vikiwa na thamani ya Sh 474,000 mali ya Said
Mrisho.
Hati hiyo ilielezwa kuwa kabla na baada
ya kutekeleza tukio hilo, mtuhumiwa huyo alimchoma, Mrisho sehemu
mbalimbali za mwili wake ikiwamo machoni, tumboni na mabegani ili
kurahisisha kupata mali hizo.
Mama mzazi wa Mrisho
Nje ya mahakama hiyo, mama mzazi wa
Mrisho aitwaye Halima Jissu pamoja na ndugu na jamaa zake walikuwa
wakilia muda wote huku wakisema wanamwachia Mungu kwa kilichotokea.
0 comments:
Post a Comment