By Mwanaspoti
KWA
muda mrefu klabu ya Yanga ilikuwa kwenye malumbano na Manispaa ya Ilala,
ikishinikiza kuruhusiwa kupewa kibali cha kujenga Uwanja wa kisasa
kwenye eneo la makao yao makuu iliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani,
jijini Dar es Salaam.
Katika
mzozo huo ilifikia mahali wanachama wa klabu hiyo kutishia kufanya
maandamano ili kulazimisha serikali kuwapa nafasi kwa madai wanajisikia
aibu kuchekwa kwa kukosa hata uwanja wa mazoezi wakati klabu yao
imezaliwa miaka mingi iliyopita.
Hata
hivyo, pamoja na vitisho vyote, Manispaa ya Ilala iliendelea kushikilia
msimamo wake ikiitaka Yanga isahau habari ya kujenga uwanja na majengo
mengine kwenye eneo hilo kutokana na ukweli eneo la Jangwani ni
hatarishi kimazingira.
Yanga
ilikuwa ikishinikizwa kutafuta maeneo ya nje ya mji kama walivyofanya
watani zao, Simba waliokwenda kununua kiwanja Bunju ama Azam
waliokimbilia mapema eneo la Mbande, Chamazi wilayani Temeke.Hata
hivyo, baada ya kutafakari kwa kina na kuangalia ukweli ulivyo, Yanga
iliamua kutuliza akili na kufanya jambo ambalo kwa makini ni kuonyesha
ukomavu na usikivu baada ya kuamua kusaka eneo huko Kigamboni.
Yanga
imepewa ardhi na Mwenyekiti wao, Yusuf Manji aliyemega sehemu ya eneo la
hekta 712 analomiliki, ili klabu hiyo ijenge uwanja wake na kumaliza
kelele zisizoisha za kushinikiza kujenga uwanja eneo la Jangwani ambako
ilikuwa vigumu kufanikiwa.
Jana
Jumatano klabu hiyo ilizindua eneo hilo kwa kuweka jiwe la msingi ili
kuanza mchakato wa ujenzi wa uwanja huo, jambo ambalo hata aliyekuwa
Mgeni Rasmi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Mama
Fatuma Karume wamesifia kuwa ni kuonyesha kwa kiasi gani viongozi wa
Yanga walivyo wasikivu na makini katika maamuzi.
Mwanaspoti
linaamini zile ndoto za muda mrefu za wanachama wa Yanga kama ilivyo
kwa wenzao wa Simba kuona klabu zao zinakuwa na viwanja vyao na
kuepukana na gharama za kukodisha zinaanza kukaribia.
Simba
na Yanga kwa muda mrefu zimekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya
kuhama kutoka kiwanja kimoja hadi kingine ili kuwezesha vikosi vyao
kufanya mazoezi, acha na kunyanyasika na viwanja vya kuchezea mechi zao
za Ligi Kuu ama mashindano mengine.
Lakini
wenzao Simba walikuwa wajanja baada ya kuwahi kununua eneo Bunju ambalo
kwa sasa linaendelea vema kwa ajili ya kukamilisha awamu ya kwanza ya
kupatikana kwa kiwanja cha mazoezi kwa ajili ya timu hiyo. Ila
kwa vile Yanga nao wamejikomboa ni wazi yale mapinduzi ya soka
yaliyoonyeshwa na Azam inayomiliki uwanja wa kisasa na hosteli zake huko
Chamazi, sasa yatahamia kwa klabu hizo kongwe za Simba na Yanga.
Kitu
cha muhimu viongozi, wanachama na wadau wa klabu hizo washirikiane
kuharakisha ujenzi wa viwanja hivyo na miradi mingine iliyokusudiwa
kwenye maeneo ya ardhi za klabu hizo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa
ubora zaidi.
0 comments:
Post a Comment