
Hiyo ndiyo sababu naweza kuhisi kile
ambacho kinamuumiza mtoto aliyetelekezwa. Mimi ni baba, najua ni kiasi
gani mtoto wangu ananihitaji kwa ukaribu. Upendo wangu kwake umekuwa
zawadi yake muhimu kutoka kwangu kuliko kitu chochote. Hivyo basi, najua
atapitia machungu kiasi gani kama nikimtelekeza.
Chukua hii; Kwa
hali yoyote ile, mzazi hana leseni ya kumtelekeza mtoto wake. Changamoto
zije na ziondoke, hakikisha unabaki umemganda mwanao. Kosa la
kumtelekeza mtoto linafanana na la kuua. Huyo ni mtoto wako, unamkimbia,
unataka alelewe na nani?
Mwanamuziki Aboubakar Shaban Katwila ‘Q
Chilla’ katika nyimbo zake Aseme na Si Ulinizaa, alionesha wazi kuumizwa
na alivyokataliwa na baba yake, Shaban Katwila, tangu akiwa mimba.
Baba
mcheza soka maarufu Tanzania, mtoto anaishi kwa shida, akisaidiwa na
wasamaria wema, wakati huo mama mzazi alishafariki dunia. Q Chilla
akaokotwa! Ukitafakari vizuri unaweza kuhisi Q Chilla aliumia kiasi
gani.
Baada ya vilio vingi, mzee Katwila alitumia njia mbalimbali
kutengeneza suluhu na mwanaye. Wakasameheana na kudumisha upendo kama
mtu na mzazi wake. Tangu hapo, Q Chilla alipitia vipindi vingi vibaya,
baba yake akawa msaada wake.
Mara ya mwisho nilipozungumza na Q
Chilla, alikiri kuwa yupo kwenye kipindi kizuri sana cha maelewano na
baba yake na kwamba alikuwa mmoja wa watu waliompigania aweze kuacha
matumizi ya dawa za kulevya baada ya kutopea.
Chukua hii; Watu
hufanya makosa lakini ni haohao hugeuka watu wazuri. Anaweza kukutenda
leo lakini kesho akakufaa. Ni mwongozo wa wahenga kuwa hupaswi kutupa
jongoo na mti wake.
Isisahaulike migogoro ya kimapenzi husababisha
maumivu mengi kwa watoto, vilevile uchonganishi kati ya mtoto na mzazi
mmoja. Mama akibaki na mtoto baada ya kutofautiana na baba yake, anaweza
kumjaza mtoto sumu kuwa baba yake alimsusa, hakumjali.
Hutokea kwa
akina baba ambao hulea watoto bila mama zao, nao hutema sumu yenye
uchonganishi kati ya mtoto na mama yake. Ni vizuri sana mtoto
anapopevuka ayapime matukio ya nyuma kwa kutumia akili ya kikubwa.
Anaweza kupata majibu ambayo ni mazuri mno kwa maisha yake.
Kwanza
mzazi ambaye anamtelekeza mtoto wake ni mtu ambaye anastahili mno
kuhurumiwa, maana hawezi kuwa sawasawa. Binadam aliyekamiliki kiakili
anatambua kuwa mtoto ni sehemu ya maisha yake, hatathubutu kumtelekeza.
Stadi
wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul Juma ‘Diamond Platnumz’ ana machungu yake.
Alishapata kueleza kuwa baba yake, Abdul Juma hakuwa na muda naye
kipindi anakua, hivyo jukumu la malezi na ukuaji wake, lilisimamiwa na
mama yake, Sanura Kassim ‘Sandra Khan’.
Malezi ya Diamond yalijaa
machozi na jasho, mama yake akihangaika huku na huko kuhakikisha mtoto
wake anapata mahitaji muhimu, japokuwa haikuwezekana kupata yote. Kwamba
wakati huo wa mateso, baba yake aliendekeza utoto wa mjini, akashindwa
kuzingatia kuwa yeye ni baba.
Diamond naye ameamua kutoa adhabu kali
kwa baba yake. Hamshirikishi kwenye mafanikio yake. Wengi tu wanakula
matunda ya kazi yake ya muziki ambayo imempa umaarufu mkubwa barani
Afrika na kwingineko duniani, baba mtu haambulii chochote.
Baba
Diamond anapigika, anaumwa anakosa mpaka msaada wa matibabu, wakati huo
Diamond anatapanya fedha kwa watu wengine. Inawezekana anafanya hivyo
kutokana na hasira kali alizonazo, ila zimezidi kipimo.
Leo hii
Diamond hana ubavu wa kumfuta baba yake kwenye mzunguko wa maisha yake,
isipokuwa atabaki kuwa baba yake anayemchukia. Na je, hizo chuki
hazifiki mahali zikaisha?
Kuna adhabu kubwa ambayo Diamond anashindwa
kuitumia, na yenyewe ni kuwa chanya kwa baba yake. Angekuwa anamjali na
kumpa huduma nyingi muhimu, angekuwa anamsuta kwa vitendo, kwamba yeye
alimtelekeza kisha anamhudumia.
Uamuzi wa Diamond kutomjali baba yake
ni kisasi. Na ni mwendelezo wa damu mbaya ambayo mara nyingi huhama
kutoka kwa mzazi mmoja kwenda kwa mwingine.
Leo hii Diamond ni baba,
yupo vizuri na mwanaye kwa sababu hakuna mgogoro kati yake na mama wa
mtoto wake ambaye pia anatarajia kumzalia mtoto wa pili. Mama ni raia wa
Uganda, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, mtoto aliyepo ni wa kike,
Latiffah, wanatarajia wa kiume.
Inaweza kutokea baadaye Diamond
akagombana na Zari kisha akawa mbali na watoto wake kwa sababu ni
wadogo. Mama akatumia nafasi yake kuwajaza sumu watoto wake kuwa baba
yao aliwatelekeza. Nao wakikua wakamchukia baba yao. Diamond anatakiwa
ayapime hayo.
Huu ni wakati mzuri mno kwa Diamond kukata mnyororo wa
chuki kati yake na baba yake. Kutosikia kilio cha baba yake ambaye
anaumwa ugonjwa mkubwa (kansa), ni roho ngumu mno. Ni roho ngumu mithili
ya ile ya Jenerali Idd Amin Dada wa Uganda.
Diamond anayo nafasi ya
kumhudumia baba yake kama ambavyo mtu anaweza kujitolea kwa ajili ya
raia wengine wenye matatizo wanaomgusa. Kiusamaria wema tu. Ajitolee tu!
Namkumbusha
kuwa alimnunulia gari aliyekuwa mkongwe wa muziki nchini, marehemu
Marehemu Muhidin Maalim Gurumo, baba yake akiwa anaishi katikati ya
dhiki kubwa. Vilevile amekuwa akinukuliwa kutoa misaada mbalimbali, baba
yake anateseka. Misaada sharti ianze nyumbani.
Hiyo chuki mpaka lini
Diamond? Mbona hujakana kutumia jina lake? Unaitwa Nasibu Abdul Juma,
huyo Abdul Juma unamwacha anataabika kwa sababu ya visirani vya nyakati
za giza. Tafadhali Diamond usiwe na roho ya Idd Amin, haikufai. Zipo
baraka nyingi utaongezewa baada ya suluhu yako na baba yako.
Imeandikwa na Luqman Maloto
sidhani kama ni kweli huyu baba ni halisi kwa Dimond kwa sababu zipo stori zingine zinasema kwamba hiyo mimba ya Dimond aliikuta. vyovyote vile lakini simtetei diamond hapa, kama kweli huyu baba hakutoa malezi kwa mtoto na mtoto akapata tabu ya maisha wakati akiona kabisa kwamba baba anauwezo wa kunitunza, na kama mateso au manyanyaso hayo aliendelea kuyatoa mpaka wakati diamond anakuwa na akayaona kwa macho yake na kuyatambua... sasa inategemea yalikuwa ya namna gani. inaweza ni makubwa ambayo si rahisi hata kuyatamka mbele za watu inabaki kuwa siri ya mama mtoto na baba, na inawezekana kabisa kwa hekima tu diamond au mama yake hawayaki wazi. kwa hiyo tusimlaumu sana, na ukiona hivyo mtoto harudi nyumba kabisa Amini kuna kitu kizito si mateso au manyanyaso ya kawaida. na ndio maana Diamond anaendelea kufanikiwa sababu huyu mzee alichokifanya kwa mtoto hata Mungu hakukipenda, na Mungu kamfanikisha kusudi Diamond ili huyu mzee apate adhabu yake hapa duniani kulingana na mateso au kosa alilofanya kwa mwanae. kwa hiyo sisi tuseme tusemavyo na huyo baba aombe kuonewa huruma kwa nguvu zake zote lakini Mungu na wahusika ndio wanajua kuna siri gani. tuache kumlaumu Diamond KUNA KITU. HASINGEWEZA KUWA NA ROHO NGUMU HIVYO.
ReplyDelete