Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imewasilisha marekebisho ya
Katiba ya Zanzibar ya 11 ya mwaka 1984, ambayo yatatoa nafasi na kumpa
uwezo Rais wa Zanzibar, kuchagua wajumbe wa Baraza la Wawakilishi bila
ya kushauriana na Kiongozi wa Upinzani ambaye kwa sasa hayupo katika
baraza hilo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria,
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, katika
marekebisho hayo vifungu viwili vinahitaji kufanyiwa marekebisho
kikiwemo cha 66 kwa kufanya marekebisho na kufuta maneno ya vyama na
kiongozi wa upinzani.
Akifafanua katika kifungu hicho, alisema lengo lake ni kutoa nafasi
kwa Rais wa Zanzibar kuchagua nafasi mbili za wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi bila ya kushauriana na Kiongozi wa Upinzani katika Baraza
ambaye kwa sasa hayupo, baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kususia
Uchaguzi Mkuu wa marudio mwaka huu, na hivyo kutopata mwakilishi yeyote
na hivyo kufutika kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo Katibu Mkuu wa
CUF, Maalim Seif Shariff Hamad alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Haroun alisema katika mazingira ya sasa katika Baraza la
Wawakilishi, hakuna kiongozi katika Baraza hilo pamoja na vyama
vilivyopata wingi wa kura, hatua ambayo imemfanya Rais kushindwa kuteua
wajumbe wawili katika Baraza la Wawakilishi.
‘Katika Baraza la Wawakilishi la sasa Rais ameshindwa kuteua
wajumbe wawili katika nafasi kumi ambapo anatakiwa ashauriane na
kiongozi wa upinzani ambaye hayupo kwa sasa,” alifafanua na kuongeza
kuwa Kifungu cha 77(2) kinafuta neno la upinzani lenye uwakilishi ndani
ya Baraza la Wawakilishi.
Akifafanua, alisema marekebisho ya Katiba yanayopendekezwa mbele ya
Baraza la Wawakilishi, lengo lake kubwa kuimarisha demokrasia na kumpa
nafasi Rais kuchagua wajumbe wa Baraza watakaofanya kazi kwa maslahi ya
taifa.
Katiba ya Zanzibar imempa mamlaka Rais wa Zanzibar kuchagua wajumbe
10 katika Baraza la Wawakilishi, ambapo nafasi mbili kwa kushauriana na
kiongozi wa upinzani ambaye hayupo kwa sasa.
Wajumbe watatu wa Baraza la Wawakilishi walioteuliwa kutoka katika
vyama vya upinzani, wanatokana na nafasi 10 kwa mujibu wa uwezo aliopewa
Rais na Katiba. Wajumbe hao watatu kutoka vyama vya upinzani ni Hamad
Rashid Mohamed, Juma Ally Khatib na Said Soud Said.
0 comments:
Post a Comment