,./.,

,,

... ...

';';';';

''=

==

adv
Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Monday, November 23, 2015

<br />
<br />
Rais Dk. John Pombe Magufuli

Rais Dk. John Pombe Magufuli
Ni dhahiri kwa sasa macho, masikio na mawazo ya Watanzania yameelekezwa kwenye uundwaji wa Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli. Shauku na matarajio juu ya sura zitakazokuwamo kwenye Baraza la Mawaziri pamoja na watendaji wengine, vinatokana na kujipambanua vilivyo kwa Dk Magufuli pamoja na timu nzima ya CCM wakati wa kampeni za uchaguzi.

Lakini, shauku na matarajio ya wengi vinajengwa na kuona utekelezwaji wa dhana ya mabadiliko iliyotumiwa kwa nguvu na wagombea wengi katika kampeni za uchaguzi.


Pamoja na kuwa serikali ya awamu iliyopita ya Rais mstaafu, Dk Jakaya Kikwete ilijitahidi kutelekeza ilani ya CCM, ni ukweli usiopingika kuwa baadhi ya watendaji walichangia kukwama kwa utekelezaji wa majukumu ya Serikali hiyo.



Hali hii ilisababisha chama tawala kufanya jitihada za makusudi ili kurudisha imani iliyoanza kupotea miongoni mwa wananchi. Jitihada hizo ni pamoja na ziara zilizofanywa nchi nzima na viongozi wake wakiongozwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana. Katika ziara hizo, Kinana alidiriki kuwataja kwa majina watendaji wakiwamo mawaziri ambao aliwaita “mizigo”.






Sababu ya ushindi kiduchu
Ushindi wa asilimia 58 ambao CCM imeupata katika uchaguzi uliomalizika ni ishara nyingine inayoonyesha kuwa wananchi walipoteza imani na utendaji wa baadhi ya viongozi wa Serikali iliyopita.


Sote tulishuhudia namna ambavyo chama tawala kililazimika kutumia uwezo wa ziada wakati wa kujinadi kwa wapiga kura. Wachambuzi wa mambo ya siasa wanaeleza kuwa ushindi wa kiwango hicho wa CCM umetokana na wananchi kuchoshwa na kuboronga kwa watendaji, na wengine wanaeleza kuwa utendaji wa Dk Magufuli wakati akiwa ni waziri ulisaidia kupatikana kwa sehemu kubwa ya idadi ya kura ambazo CCM ilijipatia.



Katika hali yoyote, kufuatia changamoto hizo, ni wazi kuwa Dk Magufuli ana kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa anakidhi shauku na kujibu matarajio ya walio wengi (wakiwamo wapinzani wake kisiasa) kwa kuunda Serikali yenye watendaji wachapakazi.



Yeye mwenyewe amesikika mara kadhaa akitoa ahadi ya kutowaangusha wananchi, lakini pia akitoa onyo juu ya kutowavumilia watendaji wazembe. Katika fasihi na maandiko ya usimamizi wa umma (public management), tafiti kadhaa zimetumia modeli maarufu ya matarajio-kutothibitishwa au kwa Kiingereza expectancy-disconfirmation (E-D) model ya kuridhika kwa wananchi juu ya huduma za umma.



Modeli hii ya E-D inaonyesha kuwa wananchi hupima huduma za umma siyo kwa kiwango cha uzoefu kwenye ubora wa huduma hizo, bali kwa kulinganisha ubora wa huduma hizo na matarajio yao ya awali. Hii ndiyo hali inayoakisi shauku na matarajio ya uundwaji wa Serikali ya Awamu hii ya Tano.



Pamoja na ukweli kuwa ni jambo lisilowezekana kwa Dk Magufuli kufanya uteuzi wa watendaji wote wapya, lakini kwao shauku kuu na matarajio ni kuona sura nyingi mpya ambazo hazina rekodi mbovu ya utendaji.




Tunataka utendaji



Kiu ya wananchi wengi kwa sasa ni kuona kuwa uzembe, ufisadi na kero nyingine nyingi za muda mrefu zilizotokana na utendaji wa Serikali iliyopita zinatatuliwa mara moja na Serikali itakayoundwa. Kuna kundi kubwa pia la wananchi ambao wana shauku na matarajio juu ya uchukuliwaji wa hatua kwa makosa mbalimbali ya kiutendaji yaliyofanywa na baadhi ya watu katika Serikali iliyopita.



Ukimtazama Dk Magufuli unaweza kukubaliana kwamba kwake usemi wa Kiswahili kwamba ya kale hayanuki haupo. Hii inatokana na jinsi ambavyo amekuwa akijipambanua katika kampeni za uchaguzi, lakini pia, kwa kuziangalia siku chache za utekelezaji wa majukumu baada ya kuapishwa kwake.



Katika hatua nyingine, kuna uwezekano kuwa yeyote ambaye atateuliwa katika Serikali ya Dk Magufuli hatataka kufanya uzembe ili kuifanya kivitendo dhana ya hapa kazi tu ambayo imekuwa ikitumika na Rais kudhihirisha mkakati wa Serikali yake.



Ni lazima watendaji watakaoteuliwa kukubali kwenda sambamba na kasi ya utendaji wa Dk Magufuli ambaye ameionyesha mara nyingi akiwa waziri, kiasi cha kupachikwa jina la utani la tingatinga. Ni dhahiri hali hiyo itasababisha wananchi wakidhi kiu yao kutokana na kupatiwa jibu la matarajio yao.



Hii itasaidia pia kurudisha imani yao kwa CCM na kujiandalia mazingira mazuri ya ushindi katika uchaguzi wa mwaka 2020. Tofauti na hali hii, CCM itakuwa inajichimbia kaburi lake yenyewe, jambo ambalo haiyumkini Rais Dk Magufuli mwenyewe pamoja na makada wa CCM hawalihitaji.



Waswahili wanasema siku hazigandi. Umewadia sasa ule wakati ambapo shauku na matarajio ya wananchi vitajibiwa kwa Rais Dk Magufuli kufanya uteuzi na kukamilisha safu ya watendaji watakaosaidiana naye katika utekelezaji wa ilani ya CCM na kutimiza ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi.


0 comments:

Post a Comment

ufunguzi