Uchunguzi
wa awali kuhusu ajali ya chopa iliyogharimu maisha ya aliyekuwa mbunge
wa Ludewa, Deo Filikunjombe na wenzake watatu, unaonyesha ilitokana na
hitilafu ya injini,
Katika
ajali hiyo iliyotokea Oktoba 16 kwenye pori la Selous, mbali ya
Filikunjombe, rubani wa chopa hiyo, Kapteni William Silaa na wengine
wawili waliokuwamo ndani ya chombo hicho kilichokuwa na namba za usajili
5Y-DKK na namba za
utengenezwaji 7027 Eucereuil, pia walifariki dunia.
utengenezwaji 7027 Eucereuil, pia walifariki dunia.
Filikunjombe
alikodi chopa hiyo kutoka kampuni ya ndege ya Sun Drew inayomilikiwa na
aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka na ilikuwa
inafanyiwa ukarabati na kampuni ya Laid Loris.
Baada
ya ajali hiyo Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa
ushirikiano na Wizara ya Uchukuzi waliita timu ya wachunguzi wa ndege
kutoka Ufaransa ambayo ilitua nchini Oktoba 20. Timu hiyo ya watu wanne
ilijumuisha mtu mmoja kutoka kampuni ya Airbus Industries ya Marseilles
ambao ni watengenezaji wa chopa hiyo; mtu mmoja kutoka kampuni ya Turbo
Meca, waliotengeneza injini; na watu wawili kutoka BEA, kitengo cha
uchunguzi wa ndege kutoka Serikali ya Ufaransa.
Timu
hiyo ilibaini hitilafu hiyo, ikibainisha kuwa baada ya injini kufeli,
chopa hiyo ilianza kushuka hadi ikaanguka na kulipuka. Sababu za
kulipuka kwake zimetajwa na wachunguzi hao kuwa ni madumu matano ya
mafuta ya ujazo wa lita 20 yaliyokuwa ndani ya chopa hiyo.
Mchunguzi
Mkuu wa Ajali za Ndege wa Wizara ya Uchukuzi, Omar Mhina aliiambia
Mwananchi kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni
kufeli kwa injini.
“Katika
uchunguzi wa awali, tulichukua injini na kugundua kuwa ilipata
hitilafu. Hiyo ndiyo lugha ya kwanza tunayoweza kusema wakati tukisubiri
uchunguzi mwingine,” alisema Mhina katika mahojiano na Mwananchi.
Mhina
alisema wameshaichukua injini kutoka pori hilo la Selous na kwamba
wanatarajia kuipeleka kwa watengenezaji wake kwa ajili ya kufunguliwa na
kujua kiini cha kufeli kwa injini hiyo.
Alisema
waliwasiliana na wamiliki wa chopa hiyo nchini Kenya, lakini hawajapata
ushirikiano wa kuridhisha mpaka sasa. Lakini Mwananchi ilizungumza na
opereta mkuu wa chopa hiyo wa Kenya, na rubani wa kampuni ya Sun Drew,
Kapteni Charles Wachira ambaye alisema TCAA hawajawasiliana na Mamlaka
ya Anga ya Kenya (KCAA) kwa ajili ya uchunguzi wa ajali hiyo.
“Mimi
ni kapteni wa ndege lakini siwezi kufanya lolote kama sijapata baraka
kutoka TCAA na KCAA. Wao ndio walitakiwa wawasiliane kwanza kabla ya
sisi Sun Drew kuchukua hatua zozote, ni suala baina ya serikali na
serikali,” alisema Wachira.
Kapteni huyo amesema akipata ruhusa kutoka KCAA atakuja nchini kwa ajili ya uchunguzi wa chanzo cha ajali ya chopa hiyo.
Kauli ya Musyoka
Lakini
Kalonzo alisema kampuni yake imeshampa baraka zote, Kapteni Wachira ili
kushirikiana na Tanzania kubaini chanzo cha ajali hiyo na kwamba
kilichochelewesha ujio huo ni kusubiri kumalizika kwa shughuli za
uchaguzi zilizokuwa zikifanyika Tanzania.
Kalonzo
alisema walituma mwakilishi ambaye ni mjumbe wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, Peter Mathuki kupeleka salamu za rambirambi na kuhudhuria
msiba wa Kapteni Silaa.
“Ni
lazima tushiriki katika hili kwa sababu ni pigo kubwa kwetu na kwa
serikali yenu. Tayari Kapteni Wachira amekuja huko ili kushirikiana na
Mamlaka ya Anga ya Tanzania,” alisema Kalonzo.
Mafuta yalilipua
Chanzo kingine cha ajali hiyo kilichoelezwa na timu hiyo ni madumu matano ya mafuta ya ndege yaliyokuwa yamepakiwa ndani.
“Walikuwa
wamebeba hayo madumu yenye mafuta ya akiba kwa kuwa walikuwa wametokea
Ludewa ambako hakuna mafuta; unajua chopa hazikai na mafuta kwa muda
mrefu ndiyo maana walibeba mafuta ya akiba,” alisema mtoaji habari wetu.
Kadhalika
chanzo hicho kimesema viti vya ndege vilionekana kuanguka na kuvunjika
na watu waliokuwamo walivunjika uti wa mgongo na miguu. Hata kama
wasingeungua, wangepoteza maisha kutokana na madhara ya kuanguka kwake.
Ripoti ya BEA
Ripoti
ya awali ya Kitengo cha uchunguzi wa ajali za ndege cha Serikali ya
Ufaransa (BEA) iliyochapishwa kwenye tovuti yake imeeleza kuwa chopa
hiyo ilionekana ikianguka kutoka angani, ikiwa tayari haina nguvu na
ikifuka moshi. Kadhalika chopa hiyo ilionekana kwa muda mrefu ikiruka
umbali wa chini na baada ya kuanguka, ililipuka.
Turbomeca
Lakini
mkuu wa kitengo cha wanafizikia wa kampuni ya Turbomeca iliyotengeneza
injini ya ndege hiyo, Delpgine Robelin alikataa kutoa maelezo akisema
kuwa ni ya siri. “Hii ni siri kubwa. Hakuna taarifa zozote zinazoweza
kutolewa,” inasema barua pepe ya Robelin akijibu barua pepe ya Mwananchi
iliyoomba kupata ripoti ya awali ya uchunguzi wa ajali hiyo.
Mawasiliano angani
Uchunguzi umebaini pia Kapteni Silaa hakuwasiliana na kitengo cha usalama wa anga na mawasiliano ya ndege cha TCAA
Kuhusu
tatizo la chopa. Mhina amesema Kapteni Silaa aliwasiliana na kitengo
hicho wakati ndege ipo ardhini, ikipaa na ilipofika juu, lakini baada ya
hapo hakukuwa na mawasiliano yoyote.
“Kabla
hajaruhusiwa kwenda eneo jingine la anga (area control route) ndipo
alipokata mawasiliano na hakuwasiliana hata na ndege nyingine kueleza
kama ana tatizo,” alisema.
“Kwa
kawaida chopa zinatakiwa kuwasiliana zikiwa angani, lakini hakuna chopa
yoyote iliyotoa taarifa kama waliwasiliana na Kapteni Silaa,” alisema
Mhina na kuongeza: “Iwapo chopa ina matatizo ya injini, kuna namna
ambayo marubaini wanaweza kudhibiti ili kusitokee madhara, lakini
haijulikani kwa nini Kapteni Silaa alishindwa kudhibiti hali hiyo.”
Shahidi
Mhina
alisema kwamba mmoja wa mashuhuda aliiambia timu ya wachunguzi kwamba
alianza kuona chopa hiyo ikifuka moshi wakati iko hewani. “Lakini
haikuwa ikiungua, hapana, ilifuka moshi hadi ilipoanguka ndipo ikawaka.”
CHANZO MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment