,./.,

,,

... ...

';';';';

''=

==

adv
Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Monday, July 27, 2015

NI mfululizo wa simulizi ya maisha ya staa nguli katika fani ya uigizaji, Jacob Stephen Mbura ‘JB’. Hakika ni simulizi tamu iliyojaa mafunzo, hamasa na burudani kwa baadhi ya maeneo. Wiki iliyopita, tuliishia pale msanii huyo alikubali kujiunga na fani ya uigizaji baada ya kupata ushawishi mkubwa kutoka kwa msanii Single Mtambalike ‘Richie’ pamoja na shinikizo la mama yake mzazi.
Hata hivyo, alipofika eneo walilokuwa wakifanyia mazoezi, akasikia sauti zikitokea ndani na alipochungulia, alichokiona hakutaka tena kuendelea kukitazama. Kufikia hapo akawa ameamua kufuta kabisa wazo la kufanya sanaa.
Je, JB aliona nini siku hiyo? Ungana nami hapa chini uzidi kujifunza mengi kuhusu vita ya maisha.

“Yalikuwa ni mazoezi makali ambayo licha ya kupitia mafunzo ya kijeshi, sikuwahi kuyaona mahali popote, yalinitia hofu mno,” anasema wakati akikaa vizuri kwenye kiti.

“Nikaona kama ni upotevu wa muda tu, nikalinganisha kazi yangu ya biashara ambayo ilikuwa ikiniingizia kipato na mazoezi hayo nikaona ni heri niendelee na biashara,” anasema.
“Kichwani nikaamua kwa dhati kabisa kufuta mambo hayo, nikajiandaa hoja nzito za kukabiliana na ushawishi wa Richie na mama yangu mzazi.

“Lakini waliendelea kunishinikiza kujiunga na mazoezi yao, pamoja na wakati mwingine kumtolea lugha chafu na za maudhi, lakini Richie hakukata tamaa wala kuvunjika moyo juu ya kunishawishi nifanye sanaa, sijui alikuwa akinifikiria nini,” anasema JB.

“Na hapa, ngoja niseme jambo ambalo moyo wangu unanishtaki kwao, jambo lenyewe ni kuhusu Richie,” anasema JB huku akitazama juu akiwa amekunja ndita, anavuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu.

“Katika mafanikio yangu ya maisha ya uigizaji, tena hata maisha kwa ujumla, hakika siwezi kumsahau Richie, huyu ni babu katika sanaa ya filamu, wewe mwangalie hivyohivyo tu,” anasema JB lakini awamu hii kwa sauti ya juu kabisa.
“Unajua hata jina la Ray, Vincent Kigosi alipewa na nani? Ananiuliza JB akiwa amenikazia macho na kabla sijajibu chochote, haraka sana akaniwahi na kunipa jibu.

“Ni Richie, kwa taarifa yako ni Richie. Sikiliza, kwangu mimi Richie ni zaidi ya msanii na rafiki, huyu ni mwalimu wangu, mhamasishaji wangu na hata ushirikiano wetu katika mambo mbalimbali ya kimaisha, hauishii kwenye filamu tu, hata mambo mengine,” anasema mfululizo JB.

“Richie ameendelea kuwa mtu muhimu sana maishani mwangu, hata familia yangu inalitambua hilo, namshukuru sana Mungu wa mbinguni kwa kunikutanisha na Richie, ni mtu sahihi katika safari yangu ya mafanikio, Mungu ambariki babu Richie,” anasema huku akionesha tabasamu hafifu kwa mbali.

“Basi bwana, Richie akaendelea na ushawishi wake hatimaye nikaamua tena kuanza kuigiza, nikaanza mazoezi, wakati huo kundi lao lilikuwa likijulikana kwa jina la Nyota Assemble,” anasema.

“Miongoni mwa wasanii niliowakuta ni pamoja na Richie mwenyewe, Waridi, baadaye wakaja akina Monalisa, Natasha, akina Mjomba Fujo na Seki, wengine siwakumbuki maana imekuwa ni muda kidogo,” anasema JB.
“Shughuli ikaendelea, nikaambiwa kufanya mazoezi kwa muda mrefu huku nikipewa mafunzo maalum, pamoja na mbinu mbalimbali za kuigiza, hakika nikaanza kuzoea ugumu wa mazoezi na kujikuta nikiwa mzoefu kabisa,” anasema kisha kuachia kicheko.

“Lakini pia, hapa nataka niseme jambo lingine muhimu sana kuhusu sanaa yetu, sijui katika makundi mengine lakini Kundi la Nyota Assemble, hakika lilikuwa kundi la kipekee sana,” anasema.

“Si tu kwamba tulijifunza kuigiza peke yake, lakini tulifundishwa nidhamu, heshima na mambo mengi sana juu ya maisha, kitu ambacho nakiona kwa wasanii wachanga hakipo,” anasema JB huku akionesha sura ‘ngumu’ kidogo.
Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatillia wiki ijayo kwa uhondo zaidi

0 comments:

Post a Comment

ufunguzi