,./.,

,,

... ...

';';';';

''=

==

adv
Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Wednesday, February 18, 2015

Nchini Nigeria mwanajeshi hunyongwa anapokataa kupigana dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram.
Hivi karibuni nchini Kenya ilipitishwa sheria ya usalama ambayo kama busara haitotumika inaweza kuipeleka nchi hiyo pabaya. Kenya sasa itaanza kuangaliwa na watu wa ndani na nje kwamba ni dola ya kipolisi.
Serikali za nchi hizo mbili za Kiafrika; moja iko Afrika Magharibi na nyingine Afrika Mashariki, zina kila sababu ya kupambana na kuwazuia magaidi wanaohatarisha usalama wa raia na mali zao. Lakini mara kadhaa malengo mazuri humalizikia kwa matokeo mabaya na vurugu, ikiwa uangalifu hauchukuliwi.
Pia, ikiwa watekelezaji wanakuwa wakakamavu na kutokuwa tayari kuzidurusu hatua zao kila wakati kama zinaambatana na tunu muhimu za kuheshimu utu wa mwanadamu, kuna wasiwasi kwamba hatua zilizochukuwa na Serikali za nchi hizo mbili zinakosa malengo na hazitasaidia kuondoa mzizi wa fitina wa ugaidi.
Katika kisa cha karibuni cha mashambulio ya magaidi huko Nigeria, magaidi wa Boko Haram waliwateka nyara watu kadhaa. Msemaji wa Serikali ya Nigeria alikuwa hana zaidi la kusema ila kushtushwa, kusikitishwa na kukilaumu kitendo hicho.
Baada ya shambulio hilo lililofanywa karibu na kijiji kilichoko katika Mkoa wa Kaskazini wa Borno, mambo yalibadilika na kuwa vurugu tupu. Barabara nyingi zilikuwa hazipitiki na mawasiliano kupitia simu za mikononi yalikuwa hayawezekani. Kwa hakika ilichukua siku hadi sura kamili ya tukio hilo kupatikana katika mji mkuu wa Abuja.
Inasemekana wanavijiji walikusanywa na kuhamishwa kama ng’ombe, siyo chini ya 35 kati yao waliuliwa kwa risasi. Habari nyingine zinasema wanawake na wasichana 200 walipakiwa katika malori na haijulikani walikopelekwa. Japokuwa kikundi cha Boko Haram hakijasema kwamba ndicho kilichofanya hayo, lakini mabingwa wa harakati za magaidi wanasema shambulio hilo jipya lina sura kwamba Boko Haram ndio walioufanya ukatili huo.
Idadi ya ukatili unaofanywa na kikundi hicho ambacho bila ya haki kinajigamba kinausemea Uislamu, imeongezeka hivi karibuni. Mwaka wa 2014 maelfu ya watu wasiokuwa na hatia wameuliwa huko Nigeria na kundi hilo ambalo tangu mwaka 2009 limekuwa likidai kuwako dola huru ya Ukhalifa.
Kwa mujibu wa jumuiya zinazotoa misaada, Wanaigeria milioni 1.5 wamekimbilia katika mikoa iliyo na amani au wameelekea nchi jirani kutokana na kitisho cha Boko Haram.
Jeshi la Nigeria linaonyesha limeelemewa, haliwezi kuwalinda raia na zaidi haliungwi mkono na raia. Linakosa silaha za kisasa. Maofisa pamoja na wanajeshi wao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamika kwamba hawana silaha za kutosha kuweza kukabiliana na kuwashinda wapiganaji wa Boko Haram walio na silaha za kutosha.
Silaha nyingi walizonazo Boko Haram ni zile zilizoachwa na wanajeshi wa Serikali wanaokimbia kutoka medani za mapigano. Mara kadhaa kumetokea visa vya wanajeshi wa Serikali huko Borno kukataa kutii amri za wakuu wao. Wanajeshi hao husimamishwa mbele ya mahakama za kijeshi wakishtakiwa kuwa, waoga mbele ya adui au kufanya uasi. 54 kati yao wameshapewa hukumu ya kifo.
Hata hivyo, haifikiriwi kwamba hukumu kali za kifo dhidi ya wanajeshi ‘waoga’ itaibadilisha hali ya mambo inayozidi kuwa mbaya huko Nigeria. Ingekuwa bora kuushughulikia mzizi wa tatizo hilo la ugaidi wa Nigeria.
Tatizo ni ufisadi
Kwa mfano, ule ukweli halisi wa hali ya mambo kwamba sehemu kubwa ya fedha zinazomiminwa katika majeshi ya nchi hiyo zinamalizikia katika mifuko ya viongozi wa jeshi walio mafisadi. Ni rahisi kwa viongozi wa kijeshi kuwaadhibu wanajeshi walio chini yao badala ya kuupiga vita ufisadi ulioonea miongoni mwa majenerali jeshini.
Vivyo hivyo, mabingwa wa kuchunguza masuala ya ugaidi, wana wasiwasi kuhusu nafasi ya kufanikiwa njia inayofuatwa na Serikali ya Kenya katika kupambana na wanamgambo wa Al-Shabaab walio na ngome zao Somalia. Mwezi Novemba mwaka 2015 pekee walikufa watu 64 katika nchi hiyo kutokana na mashambulio yaliyofanywa na magaidi hao. Serikali ilijibu kwa haraka na kupitisha sheria ya kupambana na ugaidi.
Rais Uhuru Kenyatta ambaye hivi karibuni alifutiwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya The Hague, ameshaitia saini sheria hiyo iliyozusha mabishano makali. Yeye hajali malalamiko yaliyotolewa na upinzani wala maombi kutoka sehemu mbalimbali za dunia yaliyomtaka asiukubali muswada huo.
Hata mshipa haujampiga, licha ya kwamba majadiliano juu ya muswada wa sheria hiyo yalizusha hali ambayo wanasiasa walikamatana mashati bungeni. Kenyatta hajatetereka. Aliwajibu wapinzani kwamba asiyekuwa gaidi hana haja ya kuiogopa sheria hiyo.
Kwa ufupi, sasa kuna sheria kadhaa za usalama huko Kenya, ikiwamo ile ambayo inaipa polisi uwezo wa kumuweka ndani mtu hadi mwaka mmoja bila ya kumfungulia mashtaka. Mazungumzo ya simu yanaweza kusikilizwa na watu wa usalama bila ya kutolewa kibali cha kufanya hivyo na hakimu. Pia, waandishi wa habari wanalazimika kupata kibali kwanza kutoka polisi kabla ya kuchapisha hadharani mada zinazohusiana na usalama wa taifa.
Inategemea namna mtu anavyozitafsiri sheria hizo. Hata hivyo, jambo moja ni wazi; nalo ni kwamba Serikali ya Kenya imeamua kufungua medani mpya ya kupambana na magaidi tena kwa ukali zaidi.
Wahakiki wanazungumzia kwamba sheria hizo zinazobana uhuru wa raia hazina haja, siyo za lazima. Watetezi wengi wa haki za kiraia wanasema tatizo hasa liko katika ufisadi ndani ya Jeshi la Polisi na kushindwa taasisi mbalimbali za usalama nchini Kenya kushirikiana pamoja na kutekeleza sheria ambazo ziko tangu zamani.
Kwa Rais Kenyatta, tatizo la Al-Shabbab si rahisi bali ni tatizo ambalo mkuu yeyote wa nchi haliwezi kumpa usingizi mzuri. Lakini hata sheria hii kali iliyopitishwa karibuni siyo suluhisho. Badala ya kuwalinda raia inaweza ikawaadhibu raia haohao iliyokusudia kuwalinda.

0 comments:

Post a Comment

ufunguzi