Mheshimiwa Rais tafadhali.

Kwa kweli umenikwaza na ninajisikia nimeumia sana moyoni na mawazo yangu yako kama sufuria lililoandaliwa kwa kupikia pilau; mchele hauwekwi yanachemka mafuata na viungo. Harufu tu kwa mbaali vya kupikwa havipikwi nimebakia kula kwa harufu. Umenikwaza kwa sababu nilitarajia safari hii na mimi ungenikumbuka kama ulivyowakumbuka na wale. Teuzi zako za hivi karibuni za wakuu wa mikoa, mawaziri, manaibu waziri na sasa wakuu wa wilaya umenifanya niamini kuwa ama umenisahau, umenipuuzia au hujaona mchango wangu mkubwa.

Mheshimiwa Rais kumbuka mimi nilikuwa na nimeendelea kuwa mtetezi wako mkubwa wa utawala wako hata pale ambapo watetezi wako wengine walipogeukua kuwa walalamikaji wako. Nimekutetea hata kwenye visivyoteteeka na hata vilivyotetereka nilijaribu kuvitetea! Nimejitahidi kwenda nao mano a mano na wale wote ambao walikuwa wakikurushia madongo au kukulaumu wewe kwa madudu ambayo yamekuwa yakitokea chini ya utawala wako. Lakini naona umenisahau.

Nimebaki na maswali mengi hata Mama Chanja amenishangaa leo sijala - anadhani nimefunga Kwaresma! au nawaunga mkono Wakristu kwenye Jumatano ya Majivu! Kumbe mwenzie nimeghafilika moyoni na kwa kweli nimekwazika. Nimejikuta niko kama yule Waziri wako fulani ambaye ulimtupa nje akalazimika kujiuzulu kwa kashfa pale Bungeni. Maneno yake yale naweza kufanya yangu; "Nimeumia sana, nimekwazika sana".

Kumbuka Mheshimiwa Rais - Dakta wa madaktari, Profesa wa Maprofesa - mimi nilikutetea tangu wakati wa ile kashfa ya kwanza kabisa; ya mapanki na ndege za Warusi. Wakati ulipojitokeza na kusema kuwa watu wetu hawali mapanki na kuwa filamu ile ya Hubert Sauper ilikuwa imelenga kukashfu jina zuri la nchi yetu. Wengine waliwaunga mkono wale watengenezaji filamu na hawakuweka uzalendo wa kutetea nchi hata ikiwa imechafuka. Nilikuwa mmoja wao wa waliosema "nchi yangu kwa ubaya au kwa uzuri". Nilitetea na niliunga mkono lile tamko la Bunge kukuunga mkono; ningepitwaje vile; nichekwe? Nilijua siku ikifika na mimi utanikumbuka.

Hata ilipokuja ile kashfa ya Richmond wakati wengine walikuwa wanajaribu kukuunganisha wewe na kashfa ile na uongozi wako mimi nilikutetea hata kichinichini. Sikutaka kabisa uonekane kwa namna fulani ni sehemu ya tatizo lile. Na Sikuishia kwenye Richmond tu; nilikutetea kwenye Poormond, Failmond ya shule zetu na hata hivi majuzi mlivyowatumia wasanii kuuza uzuri wa chama chetu/nu nilikutetea kwenye suala la Diamond!

Mheshimiwa Rais nimekutetea katika jua na mvua, baridi na joto hata ilipodibi kuupindisha ukweli a.k.a kuongopea - nilijaribu ilimradi Rais wangu ujue kuwa tuko baadhi yetu tunaokuamini uongozi wako maridhawa na kuwa kama shukrani yako kwetu utatukumbuka na sisi wengine. Kama uliweza kumkumbuka Adadi Rajab, washikaji zako wa Imma na hata yule Generali Shimbo na vijana kama kina Mrisho Gambo nilijua tu siku yangu itakuja na mimi nitakumbukwa.

Yaani umeweza kumbuka Makonda na hata yule jamaa aliyewahi kuwa Konda lakini umeshindwa kweli kunikumba na mimi? Hivi kweli unaweza kulinganisha michango yangu kwenye JamiiForums, Twitter, Facebook, Eastergram na hata Whatsap na michango ya hawa wengine? Kwa vile ni wazi nafasi hizi hazihitaji ujuzi fulani maalumu - kitu ambacho na mimi ninacho - kweli umeshindwa na mimi kunirusha mahali fulani japo angalau na mimi niwemo kwa wenye kuwemo? Yaani Makonda yumo mimi simo? Yaani jamaa wa Mpira umemkumbuka lakini mimi nisiye na masihara umenitupa?

Sasa, mheshimiwa; mimi nina pendekezo. Nitaendelea kukutetea na kuutetea utawala wako dhidi ya wale wote wenye kuutaka uonekane ni utawala wenye upendeleo, wenye kuzawadia uzembe na kulinda wabovu. Nitakutetea dhidi ya yale wote wanaotaka ukumbukwe kwa jini gani utawala wako unaweza kuliacha taifa katika hali ile ile uliyoikuta (mwamko mpya wa ujambazi! na kashfa). Nitajitahidi kukutea hata pale ambapo sera za chama zinaweza kufanywa zionekane zimefeli kwa kila kipimo nikiwakumbusha kuwa sera zetu hazijafeli kama za tawala tatu zilizotangulia; zimefeli kidogo zaidi kulinganisha na wao. Nitaendelea hivi kwani nina imani ya kwamba utanikumbuka.

Mheshimiwa umebakiwa na miezi michache tu; sasa unapowazawadia hawa wengine ambao si chochote wala lolote na hawajatoa mchango mkubwa kama wa kwangu na nyumba yangu. Unajua hadi mapazia yangu yana picha yako; wanangu wanavaa tsheti zile za uchaguzi hadi leo. Watu wanatujua kuwa sisi ni wakereketwa wa Kikwete. Kila unapoenda nje kupewa tuzo na sisi nyumbani kwangu tunafanya sherehe na tunatangazia jamii (nikitarajia neno litakufikia).

Sasa chonde ewe kipenzi chetu eh; wewe uliye na madaraka yote na mwenye uwezo wote wa kuwakumbuka unaotaka kuwakumbuka. Nakuomba na mimi unikumbuke. Ila hata kama ukinikumbuka miye inaweza kuwaletea nongwa wengine basi mkumbuke hata mke wangu. Unajua naye anakupenda sana wakati mwingine hadi mwenyewe nasikia wivu sijui anakupendea nini. Ila nna uhakika ukimkumbuka na yeye basi na miye nitahemea humo humo si umewakumbuka na wake za wenzangu wengine hata ubalozi. Mama Chanja anasema hata ukimpa Ubalozi wa Zimbabwe atashukuru!

Ninachokuomba na mimi unikumbuke. Unikumbuke na mimi nisije kuadhirika. NImekuwa mwaminifu sana kwa utawala wako kiasi kwamba hata wapinzani wamejaribu kuninanga sana lakini wamekwama. Naomba unikumbuke ili niwakate kizabizabina kabla hujaondoka maana ukiondoka ikifika Oktoba. Sisi wengine tutaumbuka.

Na kimbelembele chetu cha ushabiki.


Ni Mimi Mkosaji