KWAKO
Mkurugenzi wa Benchmark Production, Rita Paulsen. Bila shaka u-mzima wa
afya na unaendelea na shughuli zako za kila siku za kulijenga taifa.
Ukitaka
kujua hali yangu, mimi sijambo. Mzima wa afya na ninaendelea na
majukumu yangu ya kila siku. Nimekukumbuka leo kupitia barua, maana
kitambo kidogo hatujakutana ana kwa ana kikazi.
Nimekukumbuka Madam
sababu natambua uwepo wa shindano lako kubwa la Bongo Star Search.
Msisimko wake ni mkubwa na ndiyo maana Watanzania huwa wanalifuatilia
kwa ukaribu pale linaporindima nchi nzima.
Big up kwa mchango wako
maana mbali ya mshindi kupatikana na kupata chapaa, huwa kunakuwa na
burudani nzuri hususan kutoka kwa washiriki ambao hugeuka kuwa ‘komedi’
kutokana na vituko vyao. Pamoja na kukupa pongezi hizo lakini pia nina
jambo nataka kukukumbusha. Kwa kuwa mwaka jana shindano hilo
halikufanyika kwa kile ulichokiita kuwa ni ucheleweshwaji wa taarifa za
wadhamini kutoshiriki, umeeleweka lakini swali ni kwamba., mwaka huu je
umejipangaje? Jibu najua unalo.
Wakati
ukitafakari juu ya ujio wako mpya, ni vyema pia ukatafakari pia juu ya
ufanisi kwa kujifunza kupitia mashindano ya miaka iliyopita. Changamoto
zote, malalamiko yote uyafanyie kazi.
Watu wanataka kuona burudani na mshindi anapatikana kihalali.
Wanataka kuona kweli yule mshindi ambaye ana sifa za kuwa mshindi ndiye
anayevishwa taji. Najua pengine kutokana na majukumu yako, yawezekana
usiwe unayasikia malalamiko yote yanayoibuliwa na wananchi huku mitaani
ila usijali nitakufikishia maana mimi ni balozi wao.
Kelele za
watu wengi huwa ni mshindi kuwa tofauti na yule ambaye wengi wanaamini
ana uwezo. Jitahidi sana hilo lisitokee mwaka huu. Jitahidi kusimamia
majaji wasipendelee. Wampate mshindi ambaye kweli ana vigezo vya kuimba
na asije hata kukuangusha, awike kimuziki na si kupotea mara tu shindano
linapomalizika.
Kama unaona kuna udhaifu katika majaji ni vyema
ukawashirikisha wataalam kutoka Balaza la Sanaa Nchini (Basata) ili
waweze kutoa mawazo yao kitaalam.
Kiwango cha zawadi pia huwa ni
tatizo. Kumekuwa na uvumi wa muda mrefu kwamba zawadi inayotangazwa si
ile anayokabidhiwa mshindi, hivyo ni vyema basi mwaka huu uzushi huo
ukatafuta namna ya kuufanya ufikie mwisho.
Ni bora kutangaza
zawadi ndogo lakini ikamfikia yote mshindi kuliko kutangaza kubwa halafu
kiuhalisia anapewa ndogo. Mfumo wa kupiga kura uwe wazi na kila mtu
aamini kabisa kwamba ushiriki wake katika kupiga kura una maana. Kusiwe
na chembe ya ujanjaujanja.
Kwa leo naishia hapa.
0 comments:
Post a Comment