
Iliwahi kutokea kule Temeke wakati wa tamasha moja lililoandaliwa na kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam, ambako msanii aliyekuwa akizomewa, alilazimika kumwaga pesa kwa mashabiki ili kutuliza munkari wao.
Sina uhakika kama alifanikiwa katika nia yake, lakini kilicho wazi ni kwamba watu nusura watoane roho wakati wakizigombea noti zilizorushwa.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, imetokea tena jijini Dar es Salaam, wakati nyota wa muziki wa kizazi kipya, Nasib Abdul ‘Diamond Platnumz’ alipolazimika kumwaga kiasi cha fedha kinachokisiwa kuwa shilingi milioni moja na nusu, kuwaziba midomo ‘mashabiki mbuzi’ waliokuwa wakimzomea wakati akifanya vitu vyake jukwaani!
Inafahamika kuwa mashabiki wasiojua muziki, wamekuwa wakilazimisha uhasama kati ya Diamond na Ali Kiba, kila mmoja akivutia upande wake kuwa ndiyo unaojua zaidi kuliko mwingine, wakati wasanii hao, kwa nyakati tofauti wamekuwa wakikataa kuwepo kwa bifu kati yao. Ni watu hawa ndiyo ambao wanajitahidi kuchochea moto usiowaka, ili mradi tu kuridhisha nafsi zao.
Sitaki kuingia katika mtego huo kwa sababu najua wasanii hao wawili wana tofauti kubwa kimuziki, ambayo ni mtu asiyekubali ukweli tu anaweza kung’ang’ania kuwaweka katika mizani moja.
Kuna mashabiki wa Bongo Fleva hawampendi Diamond. Hili siyo jambo baya, kwa sababu katika muziki wenye ushindani hiki ni kitu cha kutarajia. Kwa nini hawampendi, hili ni swali muhimu linalopata majibu mepesi na ya hovyo.
Diamond anachukiwa kwa wivu tu, kwa sababu anaonekana kama msanii anayepaa kimuziki wakati wenzake alioibuka nao wakitembea. Kwao, wanaona kama ana bahati, lakini wanasahau juhudi na utayari alionao katika kuwekeza kwenye kazi anayoifanya. Namna pekee ya kumuonyesha hawamkubali ni kumzomea!
Wale mashabiki waliomzomea pale Leaders Club, walikuwa wamevaa fulana zenye maneno ya Team Kiba, kwa maana kuwa ni wafuasi wa mzee wa Cinderela. Nafsi yangu haiamini hata kidogo kama Kiba aliwatuma wakamzomee, ila kwa namna moja au nyingine, wanawagombanisha vijana hawa wenyeji wa Kigoma bila sababu za msingi.
Kitendo cha Diamond kuwarushia fedha, kwangu naona kama ulikuwa ni ujumbe kwao kuwa wanaendekeza njaa, hivyo kama hilo ndilo tatizo lao, wachukue na hizo waone kama shida zinazowazunguka zitaisha!
Ndiyo maana baada ya kurushiwa fedha hizo, kudhihirisha kuwa ni kweli wana shida, wakasahau kuzomea, badala yake wakawa bize kugombea ili kila mmoja apate. Huenda moyoni Diamond alikuwa anawacheka kwa dharau, lakini nje ya jukwaa, tupo ambao tunaamini kwa sababu zozote zile, kitendo cha wasanii kurusha fedha kutokea jukwaani, mbele ya kadamnasi, siyo kitu cha kupigiwa makofi, kwa sababu ni hatari!
Idadi kubwa ya wananchi wetu ni masikini.
Wanaweza kuja katika maonyesho wakiwa wamependeza kwa maana wamevaa vizuri, lakini nyuma yao wana matatizo mengi, hasa yanayohusu fedha. Kuitupa noti ya elfu kumi hewani na kuwataka watu hamsini waigombee ni jambo hatarishi.
Tatizo zaidi linakuja jambo hili linapofanyika usiku, hasa katika muda ambao Diamond alipanda jukwaani. Ni muda ambao wanywa viroba wameshavibugia vya kutosha na hivyo kuwatupia pesa ni kuwachanganya. Ingawa hakuna ripoti za majeruhi wa kugombea pesa hizo, si vyema jambo hili kuruhusiwa kuendelea.
Wasanii wenyewe walitambue, wanaoandaa matamasha wajue.
Kama kuwatupia fedha mashabiki ni jambo zuri, kwa maana ya kurudisha sehemu ya fedha unazopata kwa jamii yako, nadhani zipo njia nzuri zaidi na zenye tija kuliko kurusha hela kutoka jukwaani. Tupeleke mahitaji muhimu kwa wazee wasiojiweza walio makambini, tusaidie kusomesha watoto yatima na hata kujenga nyumba za ibada ili watenda dhambi wapate sehemu za kutubu matendo yao!
0 comments:
Post a Comment