
Lukuvi: Wabunge wengi wamo orodha ya dawa za kulevya
- Lakini asema Serikali haiwezi kukurupuka kuwataja kwa kuwa haina ushahidi wa kutosha
Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi amesema baadhi ya
majina ya wabunge yametajwa miongoni mwa watu wanaoshukiwa kujihusisha
na biashara ya dawa za kulevya lakini Serikali haiwezi kuwataja
hadharani kwa haraka.
Majibu hayo ya Waziri Lukuvi yamekuja baada
ya wabunge kumbana na wengine wakizomea baada ya kueleza ugumu wa kutaja
majina ya washukiwa pasi na ushahidi wa kutosha.
“Serikali
haiwezi kutaja majina haraka kiasi hicho kwani inaogopa kukurupuka na
kushindwa mahakamani, hivyo lazima tuwe makini sana na jambo hilo.
Hatuwezi kukurupuka tu eti ni fulani wakati hatuna vithibitisho.
“Kumbukeni
wengine mpo humu ndani ya Bunge na tukianza wengi mtakwisha maana
katika orodha hiyo kubwa na ninyi mmo na orodha ni kubwa kweli ambayo
wakati mwingine inatakiwa umakini wa hali ya juu,” alisema Lukuvi
alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Karatu (Chadema),
Mchungaji Israel Natse.
Katika swali lake ambalo lilisababisha
kelele za kuzomea, Natse alitaka majina hayo yatajwe hadharani. Hata
hivyo, hali ilitulia baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuingilia
kati na kusema: “Hii tabia ya zomeazomea siitaki humu ndani, acheni
tabia hiyo lazima mumsikilize mtu kwa kile anachokisema kwanza lakini
mtindo huu si mzuri...”
Patashika hiyo ilitokana na swali la
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Catherine Magige aliyetaka kujua iwapo
Serikali inaweza kuwaambia Watanzania ukubwa wa biashara hiyo nchini na
kama haioni kama kuna tatizo katika ukaguzi wa abiria na mizigo katika
viwanja vya ndege na juhudi za Serikali kumaliza tatizo hilo.
Akijibu
swali hilo, Lukuvi alisema ukubwa wa biashara hiyo hapa nchini
unadhihirishwa na idadi ya Watanzania 274 waliokamatwa kati ya mwaka
2008 hadi Julai mwaka huu kwa kosa la kujihusisha na dawa za kulevya
katika nchi mbalimbali za nje.
Alisema Serikali inafahamu ukubwa
wa tatizo la matumizi ya biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya nchini
na alitaja takwimu za ukamataji wa dawa hizo katika kipindi cha kuanzia
mwaka 2000 hadi Machi, 2012.
Alisema pamoja na kukamatwa kwa
Watanzania hao nje ya nchi, wageni 31 wanashikiliwa mahabusu katika
Magereza ya Keko na Ukonga, Dar es Salaam ambao ni raia wa Iran,
Pakistan, Senegal na Afrika Kusini.
Hata hivyo, katika swali lake
la nyongeza, Magige alisema uteketezaji wa dawa zinazotajwa kukamatwa
umekuwa wa siri kiasi cha kutiliwa shaka kuwa huenda zinachukuliwa na
maofisa waliozikamata ndiyo maana hakuna uwazi.
Kuhusu hilo,
Waziri Lukuvi alisema suala la uteketezaji wa dawa hizo hauko wazi
kutokana na sheria zilizopo kutotoa nafasi ya kuteketezwa mapema kwa
kuwa zinatumika kwa ajili ya ushahidi akisema wakati mwingine hukaa
zaidi ya miaka 10.
|
0 comments:
Post a Comment