Posted by Williammalecela.com on Tuesday, October 18, 2016
 |
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Hapi Aagiza kuwekwa rumande masaa 24 watendaji 6 wa mitaa, kata na manispaa
Ni kwa uzembe na kushindwa kufanyia kazi maagizo yake
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni leo ameendelea na ziara yake katika kata ya
Mikocheni ambako ameshiriki kikao cha maendeleo ya kata (WADC), kupokea
taarifa ya maendeleo ya kata, kuzungumza na wazee wa kata hiyo na
kufanya wa mkutano wa hadhara kusikiliza kero za wananchi.
Katika
ziara yake hiyo, Mkuu wa wilaya ameagiza kuwekwa ndani kwa saa 24
Mhandisi wa Manispaa Ya kinondoni kwa kutotekeleza agizo la kufika
katika ziara yake kwa wakati ili kujibu kero zinazohusiana na kitengo
chake.
Aidha DC Hapi ameagiza pia kuwekwa ndani kwa mtendaji wa
kata ya mikocheni na watendaji wa mitaa minne ya Mikocheni kwa uzembe na
kutotekeleza maagizo waliyopewa na Mkuu wa wilaya tangu Mwezi Mei
Mwaka huu aliyoyatoa katika kikao cha watendaji wa kata za Kinondoni juu
ya uanzishwaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi.
Aidha watendaji
wa kata hiyo wanadaiwa kupewa fedha za ujenzi wa zahanati na manispaa
ya Kinondoni kiasi cha shilingi milioni 42 yapata miaka miwili sasa,
lakini bado zahanati hiyo haijaanza kujengwa. Katika ziara yake
hiyo mkuu wa wilaya alisikiliza kero mbalimbali za wananchi ikiwemo
uvamizi wa barabara, changamoto za soko la mikocheni na kero ya maji
machafu kutiririka kwenye makazi ya watu.
Akieleza dhamira yake
katika hatua mbalimbali Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni amepiga marufuku
vibanda vya kuonesha video mitaani vinavyochochea utoro shuleni na
kuporomoka kwa maadili ya watoto kwa kuonesha picha chafu za ngono.
Mkuu huyo wa wilaya amewasisitiza vionugozi na watendaji wa kata na
mitaa kufanya kazi kwa bidii na maarifa na kuepuka kufanya kazi kwa
mazoea.
"Msikae sana ofisini, nendeni mkawatembelee wananchi
mjue shida zao na mzitatue. Huo ndio wajibu wetu. Nikipata malalamiko ya
wananchi ambayo mmeshindwa kuyafanyia kazi kwa uzembe, mjiandae
kuwajibika..." alisema Hapi.
Mkuu huyo wa wilaya kesho anatarajia kuendelea na ziara yake katika kata ya Magomeni. |

0 comments:
Post a Comment