Name:  Wazee.PNG
Views: 0
Size:  243.2 KB

Baraza la ushauri la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), limeshatoa mapendekezo ya awali ya kumsaidia Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ili kumpata mgombea urais atakayekiwakilisha chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu...

Baraza hilo linaundwa na Wenyeviti na Makamu wenyeviti wastaafu. Wajumbe wake ni marais wastaafu.. Ali Hassan Mwinyi, Benjamini Mkapa, Dr. Salmin Amour, Amani A. Karume, John Malecela na Pius Msekwa...


Duru za uchunguzi zinathibitisha kuwa tayari wazee hao wameshamdokeza Rais Kikwete na Katibu wa CCM, Abdulrahman Kinana; namna ya kumaliza vyema harakati za kumpata mgombea ili chama hicho kiendelee kuwa na mshikamano miongoni mwa wanachama wake...


Mmoja wa watu mashuhuri waliozungumza na JAMHURI wamethibitisha kuwa wazee wanashauri kuwa wagombea waachwe wapambane kwenye upigaji kura ili wale watakaokuwa wameongoza kwenye vikao vya awali hasa Halmashauri Kuu, majina yao yapelekwe kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa kwa ajili ya uamuzi wa mwisho wa wanachama..


"Kila mmoja aachwe aogelee, atakayezama basi amezama," amesema mtoa taarifa wetu ambaye yupo karibu na Baraza hilo la Ushauri la Wazee...


Ushauri huo wa Wazee umezingatia historia ya CCM, hasa mwaka 2005 ambapo mmoja wa wagombea, Jakaya Kikwete, aliundiwa "zengwe" na kamati ya maadili, lakini busara za Mwenyekiti Mkapa ilisaidia kuumaliza mchuano wa wagombea kwa namna ambayo haikuibua malalamiko ya upendeleo...


Pia, wazee wanazingatia dhoruba iliyoipata CCM mwaka 2010 baada ya kupoteza viti muhimu vya ubunge kutokana na kuwaengua wanachama walioonekana kuungwa mkono na wana~CCM na wananchi wengi. Wanatoa mifano majimbo ya Iringa Mjini ambako Chadema kupitia kwa Peter Msigwa walishinda baada ya CCM kumuengua Fredrick Mwakalebela, aliyeshinda kura za maoni na kumweka Monica Mbega...


Maeneo mengine ambako CCM ilipoteza kwa kupuuza maoni ya Wana~CCM wengi ni Arusha Mjini, Bukombe na Mbeya Mjini...


Msimamo wa wazee wa CCM unatajwa kuwa chachu ya kauli za hivi karibuni zilizotolewa na Rais Kikwete na Kinana, kwa nyakati tofauti wakisema kwamba hawana mgombea kati ya wote wanaochukua fomu za kuwania urais....


Kauli za viongozi hao zinashabihiana na kauli ya aina hiyo inayorejewa mara kwa mara na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, Sadifa Hamis Juma, ya kwamba mwaka huu hakuna mgombea atakayekatwa jina kwenye Kamati Kuu. Sadifa kwa wadhifa wake ni Mjumbe wa CC...


Julai 8 kitafanyika kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili. Julai 9 ni siku ya kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa; Julai 10 kutakuwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa. Mkutano Mkuu wa Taifa ni Julai 11 hadi 12...


Mkutano Mkuu ndio unaochagua jina la mwanachama mmoja atakayekiwakikisha chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu wa oktoba.


Chanzo: JAMHURI.... 16.06.2015