Muswada wa sheria ya makosa ya
kimtandao ya Tanzania (Cyber Crimes Act 2015) ni ‘draconian law’ ambayo
kiuhalisia imechelewa sana kuja hasa kutokana na maendeleo hasi na chanya
ambayo ni makubwa kwa nchi yetu ya “dunia ya tatu”. Ni jambo la hatari mno kwa
taifa changa na masikini kuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya teknolojia ya
mawasiliano bila kuwa na sheria ambayo itasimamia usalama wa watumiaji na
ustawi wa nchi kwa ujumla. Muswada huu unaainisha makosa yanayohusiana na
matumizi ya mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, kuweka
utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kieletroniki.
Watu wengi wamejitokeza kuupinga
mswada huu ambao umeshasainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Sheria hii itakuwa ikitumika kuanzia bara na visiwani huku ikijaribu kusimamia
makosa ambayo yanaweza kutokana na matumizi mabaya ya mitandao.
Watu wengi wamejitokeza kuipinga
hasa wale “wanaharakati” wenye imani ya haki ya mtu kuzungumza au kupata habari
bila vikwazo. Hali kadhalika tulishuhudia watetezi wa haki za binadamu
pamoja na wawakilishi wa watumiaji wa Mtandao wa intaneti nchini wakitoa sababu
zenye “uzito” za kwanini sheria hii ipite kwa hati ya dharura na bila ya kupata
majibu. Wakaendelea kuwa Muswada huu ambao kati ya “makosa” mengi
uliyonayo kubwa moja wapo ni majukumu makubwa aliyopewa Mkuu wa Kituo chochote
cha Polisi kuwa na uwezo wa kupekuwa na kuchukua vielelezo/data pale anaposhuku
kuna suala la uhalifu unaohusu mtandao.
Kiukweli nimeshangazwa sana na
hawa wanaharakati wa hii nchi,woga wa hii sheria unatokana na nini? Hii nchi
inatakiwa isimamiwe,ilindwe na istawishwe kwa gharama yoyote hata kwa kuathiri
baadhi ya maslahi ya vikundi mbalimbali vya kijamii. Inabidi tukubaliane kwamba
nchi kwanza,amani ya nchi na ustawi wake unatakiwa kulindwa kwa asilimia mia
moja bila kujali maslahi ya “wanaharakati” wa kiafrika ambao wapo kwa ajili ya
kusimamia maslahi ya wafadhili wao ambao ni mataifa kutoka nje.
Kuna ubaya gani wa kukamatwa kwa
mtu anaye sambaza taarifa za uongo,uchochezi na udhalilishaji? Ni nani asiyejua
madhara ya taarifa za uzushi kwa jamii? Kwa nini tusikubaliane kuwa
tunahitajika kuwa wakweli katika utoaji taarifa zetu kwa manufaa ya nchi yetu?
Nini umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya mawasiliano kwa mtanzania wakati
zaidi ya asilimia themanini ya mawasiliano yetu ni yale yasiyo zalishi
(Non-Productive)? Nchi iliyojaa blogu za picha za ngono na mapenzi,habari za
uzushi na zenye kashfa,matusi na zisizo na maadili kwa nini sheria hii sio
muhimu? Watu wanatumia majina yasiyo yao (fake) kwa ajili ya kutukana
wenzao,makundi mbalimbali katika mitandao kwa ajili ya kutumiana picha za uchi
na udhalilishaji,kweli hii sheria haina umuhimu kwa hili? Nchi hii ina blogu
ngapi zinazohusu maswala ya Uchumi kama
Kilimo,Uvuvi,mazingira, Ufugaji na kadhalika? Kwa nini huu usiwe mwanzo wa
kuhamasisha uanzishwaji wa blogu na makundi mbalimbali ya mtandaoni yenye dhima
chanya ya kimaendeleo? Kwa nini watu hawazungumziii kuhusu umuhimu au uzuri wa
hii sheria?
Nchi hii imegeuka ya watu
kulalamika kila siku,watu wanalalamika kuhusu mkuu wa kituo kuwa na haki ya
kuchunguza kifaa chako kama komputa hasa pale anapokutilia shaka bila hati ya
mahakama,ubaya wa hii sheria ni nini kama wewe ni msafi na hauna makosa? Ni
vipi kama kifungu hiki kinasaidia
kukamata magaidi wanaojiandaa kulipua eneo fulani hapa Tanzania hasa baada ya
kutiliwa shaka? Itakuwa yenye msaada au la? Kwa nini tupo katika mawazo hasi
muda wote? Kwani tukienda nchi za watu huko hawatukagui? Mbona hatulalamiki? Ni
watumiaji wangapi wa mitandao wanatumia hii kama ni fursa katika maendeleo? Sheria
inahusu wale wenye nia ya kufanya makosa,kwa nini uwe muoga? Kama unaipenda
nchi hii na huna maslahi binafsi basi huna sababu ya kuipinga sana sheria hii
maana hakuna anaye kataa kuwa haina mapungufu lakini inaweza kuwa mwanzo mzuri
wa kuelekea kwenye maendeleo mazuri ya matumizi ya mitandao.
Watu wanatakiwa watambue kuwa
matumizi mabaya ya mitandao yanaweza kusababisha maafa makubwa kama tulivyoona
katika nchi mbalimbali za Afrika kama Rwanda, Burundi,Afrika ya Kusini na nchi
nyingine nyingi ambapo,usambazaji wa taarifa za uongo na au chochezi
ulisababisha mvurugano na upotevu wa amani kwa takribani zaidi ya miongo miwili
sasa wanahangaika kukaa vikao kurudisha hiyo amani. Tukubaliane kuwa “Freedom
of Speech” ni muhimu sana kwa nchi ila amani,ulinzi na ustawi wa nchi ni muhimu
zaidi kuliko hiyo “freedom of speech” ya baadhi ya makundi ya watu.
Pia najua kuwa mataifa makubwa
duniani hususani ya Ulaya na huyo Marekani, hawatafurahishwa kabisa na sheria
hii kwani wao Uhuru wa habari ni muhimu kuliko ustawi au usalama wa nchi. Kwao
ni bora nchi ya kiafrika iwe na machafuko,njaa, magonjwa au umaskini wa kutupwa
kuliko kukosa “freedom of Speech” hata kama inahatarisha uhai wa Taifa.
Tumejionea mengi,wakijitahidi kuwafadhili “wanaharakati wetu” katika kupigania
mambo mbalimbali ambayo wao wananufaika au ina maslahi kwa namna moja au
nyingine.
Tupiganie nchi yetu ipate taarifa
sahihi na salama kwa ajili ya ustawi wa nchi na sio bora habari ambazo zinaweza
kuleta machafuko katika nchi yetu. Tungependa kuwa na vikundi, magazeti, tovuti
na blogu zinazotupa taarifa sahihi na zenye kujenga kama kilimo bora, uvuvi
salama na jinsi ya kuondoa umaskini katika jamii yetu na sio taarifa za picha
za uchi,maiti,chochezi,uongo wenye nia ya kugombanisha watu na kuondoa kabisa
hali ya utulivu. Watu wajifunze kuwa na nidhamu ya kuishi,nchi kama
Korea,Indonesia,Malaysia, China na nyinginezo zimeweza kudhibiti makosa
mbalimbali ya kimtandao ambayo sasa yameshika hatamu na kufanikiwa kutumia
mitandao kwa faida ya watu na jamii kwa ujumla.
Ndugu mtanzania jiulize,kwa siku
unapokea ujumbe mara ngapi? Ni asilimia ngapi ya ujumbe ni wa maana ambao unakuwa
sahihi na wenye kujenga? Ni vikundi vingapi vya kwenye mitandao tulivyonavyo
vinakuwa vikizungumzia mambo mbalimbali mazuri wa mustakabali wa Taifa letu?
Sheria imekuja kuleta nidhamu ya sisi katika kutumia mitandao kwani ukiacha
unafiki utakubaliana nami kuwa tumekosa nidhamu katika matumizi ya mitandao na
tunahitaji mahala pa kuanzia,japo sio pakamilifu lakini yatupasa kukubaliana
kuwa sharti tuanze kama msemavyo “better late than never”.
Hivyo basi,hebu tuache
kudanganyana na tuisome sheria kwa uzuri, nimechoka na wizi wa mitandao na
benki zetu,pia Sheria hii haina tofauti na sheria za nchi nyingine,sisi hatuko
kisiwani,tunaishi na wahalifu hivyo tunahitaji sheria kali kwa ajili ya
kujilinda kwa manufaa yetu kisiasa,uchumi na jamii. Usifuate mkumbo na kuishia
kutafuta vifungu vichache kwa ajili ya kukosoa kwa maslahi yako binafsi na
kuacha vingine vyenye nia ya kujenga.
Mwandishi Thabithy Bashiri
anapatikana kwa thabeethy@gmail.com
+255 717 451213
0 comments:
Post a Comment