kesi ya Zitto kabwe kupitiwa upya na Jaji Kiongozi, Shabani Lila
Sakata la kufukuzwa uanachama kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe (Chadema), limechukua sura mpya baada ya Jaji Kiongozi, Shabani
Lila kuitisha jalada la kesi yake hali inayoonyesha kupitiwa upya kwa
kesi hiyo.
Wiki hii Mahakama Kuu ilitupilia mbali ombi la Zitto
la kutaka Kamati Kuu ya Chadema kutomjadili na hatimaye kumfukuza
uanachama wake baada ya makada wenzake, Samson Mwigamba aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha na
Profesa Kitila Mkumbo kufukuzwa uanachama Desemba 2013.
Akieleza hukumu hiyo hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa
Sheria wa Chadema, Tundu Lissu, alisema kutokana na hukumu hiyo na
kulingana na Katiba ya chama chao, Zitto amejifukuzisha uanachama.
Hata hivyo, akizungumza na MTANZANIA jana, Zitto alikiri kuwa na
taarifa za jalada lake kuitishwa kwa Jaji Kiongozi huku akimtaka
mwandishi kuwasiliana na wakili wake.
Mmoja wa mawakili wake,
Emmanuel Mvula, alisema taarifa za jalada kuitwa kwa Jaji Kiongozi
alizipata jana alipokwenda mahakamani kuchukua hukumu ya kesi hiyo.
“Tangu Mahakama Kuu imetoa hukumu tumekuwa tukifuatilia hukumu ikiwa
pamoja na kulipia. Baada ya kulipia ilitakiwa hukumu hiyo ipitiwe na
mwenendo mzima wa kesi pia uchapwe. Leo nilipokuja kuchukua hukumu
nikaambiwa siwezi kupewa kwa sababu jalada limeitwa kwa Jaji Kiongozi,”
alisema Mvula.
Alisema kuna kasoro nyingi zilizojitokeza katika kesi hiyo hali inayotia wasiwasi uhalali wa hukumu hiyo.
“Kuna walakini mwingi katika kesi hiyo, kwa sababu kwa mara ya kwanza
ilitajwa Novemba 12, 2014 na ilisikilizwa na Msajili wa Mahakama kwa
sababu Jaji (John) Utamwa alikwenda kwenye mkutano,” alisema Mvula na
kuongeza:
“Iliamuliwa kuwa kesi itasikilizwa tena Machi 12. Kuanzia
hapo hatukuelewa kilichoendelea tena. Lakini kumbukumbu zinaonyesha kuwa
kesi ilitajwa tena Februari 25 na uamuzi umefanyika Machi 10 bila sisi
kuwapo.”
Alisema kuna utata wa jinsi wakili wa Chadema, Peter Kibatala alivyopata wito wa mahakama bila wao kuupata.
“Mahakama ilimwagiza Kibatala kutuandikia barua ya wito, lakini
hakutufikishia barua kwa kuwa barua yenyewe haionyeshi saini yetu ya
kupokea,” alisema Mvula.
Alitaja kasoro nyingine kuwa ni
kubadilishwa kwa Jaji Utamwa aliyekuwa akiendesha kesi hiyo na kupewa
Jaji Richard Mziray bila wao kujulishwa.
“Kesi hii ilikuwa chini ya
Jaji John Utamwa, ikahamishiwa kwa Jaji Mziray, ilibidi tuwe na taarifa.
Tulidhani ikifika Machi 12 tutajulishwa, lakini haikufanyika,” alisema
na kuongeza:
“Mahakama kama chombo cha kutoa haki kwa wananchi,
lazima kiwe na uhakika na kuzingatia mwenendo wa kesi nyingine
zilizopita. Lakini kama inashindwa kuwa hivyo tutakwenda wapi?”
Hata hivyo, alisema watatoa tamko rasmi la uamuzi wao baada ya kupata
hukumu ya kesi hiyo na baada ya kuwasiliana na mteja wao Zitto.
|
0 comments:
Post a Comment